Tuesday, May 5, 2009

Milipuko ya Mabomu Mbagala Tanzania inahitaji siku ya Maombolezo

Ni tukio la kihistoria, tukio linalotisha na kuogopesha, tukio lililochukua roho nyingi za watanzania wenzetu raia wa kawaida pamoja na askari wa jeshi letu la ulinzi (JWTZ).

Vifo vya watu zaidi ya ishirini na tatu (23) kwa haraka unaweza ukachukulia ni tukio la ajali kama vile ajali za mabasi, ukalipa uzito mdogo kwa kujijengea mawazo kwamba mbona ajali za mabasi ama treni zinaua watu wakati mwingine hata zaidi ya 30.

Na ikiwa hujatembelea eneo la tukio na kuona uharibifu na wananchi wanavyoishi kwenye mahema na ukapata habari kutoka kwa wananchi wenyewe waliokuwa wakifukuzana na makombora unaweza kutokwa na machozi.

Tofauti kabisa na ajali za kawaida, tukio la milipuko ya mabomu kule Mbagala ni ajali kubwa mno tena ni kubwa kupindukia. Ajali hii sio tu imepoteza maisha ya wananchi wengi pia imeacha wananchi wengi katika hali ya ulemavu.

Sambamba na madhara hayo, tukio hili limesababisha uharibifu na upotevu mkubwa wa mali. Majumba yamebomoka na watu wameibiwa rasilimali zao majumbani. Aidha ghala la silaha limeteketea kabisa sambamba na askari kadhaa waliokuwa katika kazi eneo hilo.

Tukio hili lilileta hofu kuu katika Jiji la Dar es Salaam na Tanzania nzima kwa ujumla. Watanzania kutoka kila pembe ya nchi walikuwa wakihangaika kupiga simu kwa ndugu na jamaa zao Dar es Salaam. Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walitaharuki, na kukimbia hovyo. Maofisi yalifungwa na watu waliogopa kukaa katika majengo kule katikati ya jiji.

Jiji lilijikuta likitokewa na wakimbizi kwa muda. Watu walikimbia hovyo na wasielewe wapi wakimbilie. Wananchi walikuwa wakikimbia huku makombora yakitangulia mbele yao wakabaki hawaelewi la kufanya.

Watoto walipoteana na wazazi wao, wengine walikufa maji wakijaribu kuvuka mto kujiokoa.

Wananchi wengine walipigwa na makombora na kufa wakati wakikimbia kujaribu kuokoa roho zao. Aidha makombora yaliruka na kutwanga sehemu mbali mbali za Jiji umbari wa zaidi ya kilometa 15 kutoka kambi hiyo ya jeshi ilipo.

Tukio hili limesababisha hofu kubwa mpaka hivi sasa, hofu ambayo inawafanya kila mkazi wa eneo la Mbagala, hasa Mbagala kuu akisikia mlio mkubwa kushituka. Aidha wananchi wa maeneo husika bado wanaishi wakiwa na kiwewe na mshituko mara kwa mara.

Kutokana na ukubwa watukio hili Taifa linahitaji siku ya maombolezo. Hii ni kutokana na madhara makubwa ya kupoteza uhai wa watu wengi na madhara kadha wa kadha yaliyotokea na madhara mengine yanayotarajiwa kuendelea kutokea kutokana na milipuko hiyo.

Aidha ingependeza siku ya maziko ya askari waliokufa iwe ndio siku ya maombolezo kitaifa, bendera zipande nusu mlingoti kama ilivyo desturi ya maombolezo.

No comments:

Post a Comment