Kwa kweli tukio la mabomu Mbagala linasikitisha na kuhudhunisha. Kwa mtu mwenye roho ya kibinadamu ni dhari utahudhunika na roho yako itauma.
Lakini jambo la kusikitisha ni kuona wananchi kadhaa kutoka sehemu mbali mbali za jiji wakimiminika kwenda kutembelea eneo hilo la maafa kana kwamba watalii.
Watanzania wenzetu wameathirika, ndugu zao wamekufa, wamejeruhiwa, nyumba zao zimebomoka iweje tukawakodolee macho tu na kuondoka.
Hivi kweli tunashindwa hata kuwachukulia chupa moja ya maji masafi? Idadi ya watu wanaomiminika kwenda kuwaangalia watanzania wenzetu walionusurika laiti kila mmoja angekwenda huko akiwa na msaada wa aina yoyote kulingana na uwezo alionao nafaikiri waathirika wangejisikia kweli watanzania wenzao wanawaonea huruma.
Lakini watanzania wenye uwezo na wa kawaida wanasubiri Serikali na wahisani wachache kama vile kina Mengi, kina Manji, Vodacom ndio wakatoe msaada kwenye maafa. Huu kwa kweli sio utamaduni mzuri unaowakilisha asili na sifa ya upendo tuliyonayo watanzania.
Matajiri wengi wamejichimbia kimya kana kwamba hawapo kabisa na hali wanaona kila siku runinga zinavyoelezea hatari na tabu wanayoipata wenzetu. Jambo la ajabu watu hujitokeza haraka kusaida mambo ya mashindano ya urembo, mipira na mambo mengine mengi lakini katika tukio la maafa makubwa kama hili watu wamekaa kimya.
Mungu anatuangaliaje katika mazingira kama haya? Jamani shime tusiende kutalii kule kwenye maafa kwa wenzetu, bali tuende kuwafariji wenzetu na kuwapatia misaada ya kibinadamu.
No comments:
Post a Comment