Saturday, April 30, 2011

ASIFIWE TUTAMKUMBUKA!

ASIFIWE TUTAMKUMBUKA!

Leo ni arobaini ya Mpendwa wetu Asifiwe Ngonyani alama ya upole na upendo iliyofutika ghafla tarehe 23/3/2011 kama imefanyika ilivyopangwa.

Pamoja na kuwa mila zetu wengi zinatueleza kuwa arobaini ni kuhitimisha msiba lakini ukweli itachukua muda huzuni kufutika katika mioyo yetu, hasa kwa tuliopata bahati ya kumuona binti huyo. Tunakubali kwasababu kazi ya mungu haina makosa. Bali Asifiwe Tutamkumbuka.

Marehemu Asifiwe akiwa na baba

Kwa upande wangu nikiwa na siku kadhaa mbali na Jiji la Dar es Salaam katika Vijiji ambako network ya mawasiliano ni mtihani kidogo hali yangu ya kifikra ilikuwa tata kidogo, nahisi ilikuwa ishara ya taarifa ya kusikitisha.. nilipokuwa katika vijiji vyenye mtandao, niko bize, baadae nikaona Misscall ya Yasinta. Sikuwa na hela ya kutosha kwenye simu siku iliyofuata Simu iliita nikiwanayo mkononi nikapokea.

Tofauti kabisa na nilivyozoea napompigia au anaponipigia, habari niliyoipata ilininyong’onyesha!, Kwa sauti ya unyonge Yasinta alisema “Jacob nilikuwa nakutafuta ulikuwa hupatikani, nilitaka nikupe taarifa Asifiwe Hatunaye Tena” kwanza nilijipa moyo huenda sikuwa kwenye simu ni mawazo tu .. lakini kwanini niwaze hivyo?....ikabidi nimuulize “Unasemaji Yasinta?” .. “Asifiewa Amefariki” alirudia kunithibitishia … hatukuongea sana .. nilimwambia tutaongea .. bado nikiwa nahisi labda ni mawazo tu .. nikamtumia msg kumuuliza tena, alinijibu “ni kweli Jacob, Asifiwe Ametuacha” tuliendelea kuchati kwa muda kidogo lakini dakiki zilivyozidi nilizidi kuishiwa nguvu.. nikakata mawasiliano..maana taarifa zilikuwa zinazidi kuniumiza!

Nilikuwa namfahamu Asifiwe baada ya kumtembelea Nyumbani Ruhuwiko miezi michache baada ya kurudi Kutoka kwenye matibabu ya moyo Dar es Salaam mwaka jana.

Ktika picha ya pamoja na Marehemu Asifiwe

Kwa waliowahi kukutana na binti huyu kama kaka Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti aliyewahi kumtembelea pale Hospitali baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo, Shaabani Kaluse ambaye pia Jumamosi ya terehe 18/03/2011 alipata bahati ya kumuaga Asifiwe, na wengine waliowahi kumuona wataungana nami kuwa binti huyu alikuwa mpole, mtulivu mwenye sura ya heshima na upendo.

“Nilijikuta nikimwambia kuwa sasa anatakiwa kurudi Shule, akiwa na tabasamu pana usoni mwake alinijibu kuwa yuko tayari kurudi shule na ndipo baba yake akaniomba nimsaidie kumtafutia shule nzuri atakayosoma binti huyu” alisema Shaabani Kaluse, ambaye naungana naye mia kwa mia.

Asifiwe alikuwa na kiu sana ya kusoma, kama ilivyokuwa kwa Kaluse nilipomtembelea, katika mazungumzo alionyesha sana kiu ya kusoma, nilimuahidi kumsaidia atakapukuwa ametulia vizuri na nikampa kitabu kinachoitwa “Mpenzi wa Kweli” nilichokiandika kwa ajili ya vijana hasa wanafunzi kikizungumzia maadili na umuhimu wa kupenda Elimu. Alikipenda sana!.

Nasikitika nilichelewa kupata taarifa, nasikitika sikushiriki wakati wa msiba ila wanablog 53 kwa niaba ya wote walipata kushiriki vizuri msiba huu mzito online, wengine walitumia simu .. wengine wakaandika kwenye blog zao .. Yasinta hakuwa peke yake wakati huu mgumu.

“Dada Naomba uamini kuwa msiba huu sio wakwako peke yako ni msiba wetu sote, yaani familia ya Mzee Ngonyani na ya Mzee Mkundi au pengine na Wanablog wote wa ndani na nje ya nchi.

Ni msiba wetu kwa sababu wengi wetu tulikufahamu wewe kupitia maandishi yako katika Blog ya Maisha na Mafanikio ambapo pia tukaifahamu familia yako na familia ya Mzee Ngonyani” alisema Koero mkundi katika blog yake.

Baada ya kuongea mambo mbali mbali namna ya kumsadia asifiwe, nilipata picha na Mzee Ngonyani.

Binafsi nilitarajia kuhudhuria arobaini ya Asifiwe, lakini nasikitika nimekuwa na wakati mgumu kimajukumu. Hata hivyo leo usiku mdogo wangu anasafiri kuelekea Sweden atanifikishia Salamu zangu kwa Yasinta. Lakini pia nitakapokuwa Songea hivi karibuni nitamtembelea Mzee Ngonyani kumpa pole.

4 comments:

  1. Aksante kaka Malihoja...

    Kwa kweli msiba huu umetugusa wote.

    R.I.P Asifiwe!

    ReplyDelete
  2. Ahsante sana Jacob kwa kuweka hapa kibarazani kwako kumbukumbu hii.Ni pigo na mshtuko mkubwa sana kwa wengi...Asifiwe starehe kwa Aamni...

    ReplyDelete
  3. Kaka Chacha,
    We acha tu! ... nilikaa na Marehemu asifiwe na Mzee Ngonyani pale Ruhuwiko, Asifiwe akaniandalia Chai, tuliongea kwa muda pamoja na Mzee Nginyani .. kwakweli tumempoteza binti ambaye ni mfano mkubwa wa kuigwa na mabiti wetu..binafsi kama ilivyo kwa da Yasinta itanichukua muda mrefu kuzoea kuwa Asifiwe hatunaye tena... Astarehe kwa Amani!

    ReplyDelete
  4. R.I.P dada Asifiwe.sisi tulimpenda ila mungu amempenda zaidi.

    ReplyDelete