Friday, October 14, 2011

Baba wa Taifa Tunamthamini?

BABA WA TAIFA TUNAMTHAMINI AU TUNAMDHARAU?

DARASA ALILOSOMA NI AIBU!

Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere (1922-1999),

Rais wa kwanza wa Tanzania.


Imetimia miaka 12 tangu Mwasisi wa Taifa la Tanzania, baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere afariki dunia. Karibu kila mtanzania amekuwa akitoa sifa kemkem juu ya Mwalimu Nyerere.


Kwa uchunguzi nilioufanya haraka haraka watanzania wengi tumekuwa tukitoa sifa kwa mwalimu kwa unafiki wa hali ya juu kutokana na kuwa tunasifu bila kuiga au kufanya aliyotaka tufanye. Tumekuwa watoto watukutu na wajeuri wanaotumwa wanaitikia lakini hawafanyi.







Picha ya kwanza kushoto juu ni kaburi la baba wa Taifa, kulia ni sehemu ya Nyumba, chini nkusho barabara ndogo kuelekea nyumba ya Baba wa Taifa, kulia ni muonekano wa nyumba ya baba wa Taifa unapoikaribia. Nyumba hiyo iliyojengwa na Jeshi la kujenga Taifa katika kutambua umuhimu wa Baba wa Taifa, imejengwa kwenye mawe mawe na kufanya ugumu kupata picha ya nyumba nzima.





Baba alijenga viwanda tumeua vyote, alianzisha mashirika ya huduma mbali mbali kama vile mashirika ya usafirishaji tumeua na mengine yako taabani yanapumulia mashine. Alitunza ardhi kwa manufaa ya Watanzania wengi na Taifa hivi sasa tunauza ardhi kama karanga. Miaka Michache ijayo hata Serikali italazimika kununua ardhi kwa Wazungu, Waarabu, Wahindi, Wachina wanaoendelea kujikusanyia ardhi hapa nchini (Unaweza kulia ukifahamu ilivyo). Miaka michache ijayo Makabaila wa kigeni na wa kitanzania watakuwa ndio wenye nchi, na yale ya Zimbabwe raia kuwa watumwa ndani ya ncvhi yao yatakuwa yamekamilika kwani hata sasa yameshaanza kila kona ya nchi. Yale aliyosema Mwalimu Serikali kutumikia Wenye mali imeshaanza na miaka michache ijayo Viongozi wasipochukua maamuzi magumu yatakamilika.

Nilipokwenda kutembea kijijini kwangu nilikuta Mtanzania fulani mwenye asili ya Asia ameombakupewa hekari 400, lakini kijiji kilitoa hekari 100 na baada ya kupata hekari hizo 100 aliendelea na kampeni ya kutaka apewe zote 400. Katika hali niliyoitafsiri kuwa ni rushwa jamaa huyo amenunua nyumba pale kijijini, akafunga satellite dish na kuonyesha mpira kombe la dunia bure kwenye eneo la wazi. Nilichofanya ni kuwaambia katika maongezi yasiyo rasmi baadhi ya wananchi na viongozi wa hapo kijijini kuwa watajuta siku moja kwa kugawa radhi hovyo kwa wageni.


Pamoja na mazuri aliyotufanyia Baba wa Taifa ni Jeshi la kujenga Taifa tu ndio lililoonyesha shukrani kwa kumjengea Nyumba Nzuri pale Mwitongo Butiama. Lakini cha kusikitisha wakati jeshi la kujenga Taifa likimuenzi Mwalimu kwa kujenga nyumba ambayo hakupata bahati ya kuishi humo muda mrefu. Wizara ya Elimu imeshindwa kumuenzi Mwalimu kwa kuheshimu Madarasa aliyoanzia kupata Elimu.


Madarasa aliyosoma Mwalimu yanasikitisha na yanatia aibu, labda tusubiri matamko ya Waziri mkuu alipotembelea Musoma kama yatafanya kazi lakini ukweli ni kwamba Madarasa hayo yametelekezwa kwa miaka mingi.



Nikiwa mbele ya Darasa alilosoma Mwalimu Nyerere


pale Shule ya msingi mwisenge, Musoma mjini


Muonekano wa ndani wa darasa alilosoma Mwalimu Nyerere


kama nilivyolikuta mapema mwaka huu.


Hivi ndivyo darasa la Mwalimu Nyerere lionekanavyo


kwa mbali kidogo

“Lazima shule hii tuifanye ibebe heshima inayostahili... kama majengo yamechakaa hakuna sababu ya kuendelea nayo, jengeni mapya lakini bila kupoteza uhalisia wa mazingira hasa
katika darasa alilosoma Mwalimu kwa kuwa ni moja ya kumbukumbu kubwa ... tukae pamoja wakiwemo wabunge na wadau wengine wote ambao ukimtaja Baba wa Taifa ni lazima wawepo ili tuone tunaboreshaje shule hii,” alisema waziri mkuu Mizengo Pinda hivi karibuni.



Napenda kutoa rai kwa wahusika kuwa maagizo ya waziri mkuu yasiingie kupuuzi katika vichwa vya walioagizwa wakabomoa madarasa aliyosoma Mwalimu, huo utakuwa ni ujinga na upumbavu. Zipo teknolojia nyingi za ukarabati majengo na jengo likabaki zuri kwa kumbu kumbu za vizazi na viza.



Ni vema sasa Serikali kuu kupitia Wizara ya Elimu, Makumbusho ya Taifa, Serikali ya mkoa wa Mara, Halmashauri ya Musoma Mjini na wadau binafsi kuhakikisha kumbu kumbu ya madarasa aliyoanzia Baba wa Taifa kupata elimu yanaboreshwa na kutunzwa kwa manufaa ya vizazi na vizi.

No comments:

Post a Comment