HATUTAKI VITA!
Busara itumike:
Nyasa ilikuwa Nyasa Tangu Enzi na Enzi!
Mhe. Dr.Jakaya Mrisho Kikwete, Mhe.Edward Lowassa, Mhe. Bernad Membe na Serikali yote kwa ujumla Watanzania Hatutaki Vita. Naamini uwezo wa kuipiga Malawi tunao, na nia ya kuipiga Malawi tunayo lakini Sababu bado ina utata mkubwa. Tutaingia kwenye madhara makubwa wakati wa vita na muda mrefu baada ya vita.
Tukiingia Vitani tutawatesa wananchi walio mipakani, tutaitesa Tanzania baada ya Vita. Kwa sasa tunahitaji kutumia nguvu zaidi katika kuinua zaidi kuchumi wa Taifa letu
Tumieni busara zenu zote kuepusha vita, inapobidi Shirikisheni jumuia za Kimataifa. Wamalawi ni ndugu Zetu, Watanzania wamejaa kule, na Wamalawi wamejaa hapa.
Ushauri wangu ni huu: Itumike busara kama iliyotumika katika mgogoro wa Ziwa Victoria na mto Nile wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu kipindi kile Serikali inashughulikia Mradi Mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kuja Kahama, Shinyanga nk. Busara iliyotumika hatimaye ikazaliwa “Nile Basin Initiative”. Angalieni kama mazingira yanaruhusu, bora ifanyike hivyo!.
Ramani nyingi za miaka ya karibuni zikiwemo za kwenye Google Earth na CIA-World Factbook zinaonyesha Ziwa Nyasa lote lipo Malawi na hata jina lake linaitwa “Ziwa Malawi”, Nafikiri ndio inawapa nguvu wamalawi kuamini kuwa ziwa lote ni lao.
Lakini pamoja na kuwa Wamalawi wana madai ya mikataba ya zamani iliyofanywa na watu ambao maeneo haya hayawahusu mikataba ambayo kwa namna inavyoonekana haikuzingatia Riparian Rights (Haki ya matumizi na umiliki wa maeneo ya maji) wakati wote tukiwa hatujajitawala bado Ramani za zamani zikiwemo Ramani ya Ujerumani ya Afrika mashariki 1888. Ramani ya Ujerumani ya Afrika mashariki 1892. Ramani ya Makoloni ya uingereza 1897. Ramani ya Afrika Mashariki wakati wa Vita kuu ya kwanza August 1915 na Ramani ya Africa 1922 hazionyeshi kuwa ziwa hilo ni la Malawi na hata jina la Ziwa lilikuwa tangu hapo ni Nyasa.
Aidha Ramani nyingi zinaonyesha mipaka ya nchi zote imezunguka ziwa. Na ikiwa kwasababu Zamani nchi yao ilikuwa ikiitwa Nyasalan ndio kigezo cha Ziwa hilo lote kuwa lao basi hata sisi Ziwa Tanganyika lote lingekuwa letu kwasababu zamani Tanzania bara iliitwa Tanganyika. Swali lingine ramani nyingi za zamani hazionyeshi moja kwa moja kuwa Sehemu ya Ziwa kuwa Msumbiji, kama ilivyokuwa kwa Tanzania na Malawi yenyewe. Leo hii sehemu ya ziwa Nyasa ipo Msumbiji kwanini Malawi hawadai na upande wa Msumbiji?.
Ushauri wangu wa pili kwa Serikali: Serikali iwasiliane na taasisi za Kimataifa zinazoshughulikia Masuala ya mipaka na kujua kwanini Riparian Rights hazikuwekwa wazi na kwanini zisiwekwe wazi sasa kuepusha migogoro zaidi. Iwasiliane pia pia na CIA World Factbook na Google Earth na mifumo yote inayopotosha kujua vigezo walivyotumia kwa ramani zao na Marekebisho yafanyike kimataifa Mapema.
Ushauri wangu wa tatu: Serikali isiruhusu hotuba za kishabiki na vyombo vya habari visiandikie mambo kishabiki na Watanzania tusijadili kishabiki.
Wamalawi wanahitaji maendeleo, na sisi tunahitaji Maendeleo wote kwa pamoja tunahitaji kutumia ziwa hilo kwa maendeleo ya nchi zetu.
Aidha ni haki ya asili kabla hata ya mipaka kwa watu waishio kando ya maziwa na bahari kutumia rasilimali hiyo, maana iliwekwa pale na Mungu kwa ajili yao.
Mhe. Dr. Jakaya Kikwete ni wewe Wakati huo ukiwa Waziri wa mambo ya Kimataifa na Mheshimiwa Edward Lowassa akiwa Waziri wa maji ndio mliomsaidia Rais Benjamini Mkapa kushughulikia kwa busara hadi mafanikio mgogoro wa Ziwa Victoria na mto Nile hadi kuzaliwa kwa “Nile Basin Initiative”.
Nina Imani pia na hili liko ndani ya uwezo wenu kulimaliza kwa amani, na hatimaye kujenga udugu zaidi na Malawi. .
Makala hii ni Maoni yangu
binafsi kufuatana na Sakata linaloendelea Ziwa Nyasa.
Jacob Malihoja
DSM 9.8.2012
No comments:
Post a Comment