JANGA LA MADAWA YA
KULEVYA
SERIKALI IMTUMIE VIZURI
RAY C
Unapotazama na kutafakari kwa haraka haraka unaona kama si
tatizo kubwa, kwasababu ukiangalia huku, ukiangalia kule unaona watu wako
katika pilika pilia za maisha yao. Mimi
pia nilikuwa hivyo, sikuwahi kufikiri kuwa tatizo la madawa ya kulevya ni kubwa
zaidi ya linavyoonekana mbele ya macho ya watu. Ukweli ni kwamba tatizo hili ni
kubwa kwa uzani ambao ukiujua utaogopa.
Nilizoea kuwaona waathirika wa dawa za kulevya na kuwadharau,
leo nathubutu kusema kumbe nilikuwa nakosea sana. Natumia fursa hii kuwaomba
radhi waathirika wa dawa za kulevya wote na ndugu zao. Nasema hivi kwasababu
kwa elimu niliyoipata baadae ingawa wako wengi wanaingia kwa kupenda hata mimi,
hata wewe msomaji waweza kujikuta umeingia katika matumizi hayo bila kutegemea.
Mshituko mkubwa na tetemeko la moyo vilinipata wakati
nilipopata fusra ya kumsaidia Rehema Chalamila
“Ray C” katika kampeni zake za kuelimisha watanzania juu ya madhara ya
dawa za kulevya yeye mwenyewe akiwa shuhuda mkuu wa janga hilo.
Katika kipindi kifupi nilichokuwa na Ray C chini ya Ray C
Foundation tulienda pamoja karibu kila mahali kufanya kampeni zetu.
Tulitembelea kwenye Shule za Sekondari kuelimisha hatari iliyopo lakini
tulienda kwa waathirika wenyewe na kuongea nao.
KAtika kukutana na waathirika mmoja mmoja na vikao vingi ambavyo
tulikuwa tukifanya na ndugu hawa, na ziara zangu pale Hospitali ya Mwananyamala
nikiongozana na Ray C vilinifanya
nijifunze mambo mengi ya hatari kutoka kwa ndugu hawa mambo ambayo walipitia,
mambo ambayo yanasikitisha na hata yaweza kukuliza.
Madawa ya kulevya yanambadilisha mtu kutoka kwenye ubinadamu
wa kawaida na kuwa kiumbe mwengine ambaye anahitaji msaada kurudi kuwa mtu wa
kawaida badala ya kudharauliwa. Muathirika anakuwa katika mazingira ambayo yeye
mwenyewe hawezi kujimudu kuishi bila kuwa katika hali ile ya kupata dawa.
Nilielezwa na waathirika wenyewe kuwa siku mtu anapokosa dawa huwa anaumwa na
maumivu ya mwili huwa ni makubwa yasiyona mfano.
Aidha nilipata kufahamnu kuwa kuna namnanyingi zinaweza
kumuingiza mtu kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na lililoniogopesha ni
mbinu za wafanya biashara na mawakala wao kutengeneza soko, hapo ndipo hata mtu
ambye hakuwa anataka anaeza kujikuta bila kuelewa ameingia kwenye matumizi ya
madawa.
Rehama Chalamila “Ray C” alinipa simulizi nyingi za kusikitisha
ambazo zaweza kukutoa machozi, namfurahia sana dada huyu kwasababu ni muwazi na
ana uchungu mkubwa sana anapoona vijana wanaendelea kuingia kwenye tatizo hilo.
Anatamani kama siku moja Tanzania pasiwepo tone la dawa ya kulevya, anatamani
kuona siku moja Tanzania hakuna muathirika hata mmoja, anatamani kuona Tanzania
siku moja hakuna mtu ameingiza dawa hata mmoja.
Nakumbuka tulipokuwa Mbeya wakati wa maadhimisho ya siku ya
kupambana na madawa ya kulevya Dunia, juni mwaka 2014, Ray C alikuwa kivutio cha
wengi, na banda letu lilivutia sana wageni kwasababu ya Ray C lakini hilo si
kubwa, Ray C alipopanda jukwaani kutoa ushuhuda wake, Aliliza watu. Ingawa mimi
mwenyewe ndio nilimwandikia hotuba yake ya ushuhuda taratibu kadiri
alivyoendelea kueleza nilijikuta nikitokwa na machozi.
Ushuhuda wa Ray C unaumiza kwani hata wakani nilipokuwa
nikiandika nilikuwa naumia sana, na hata wakati akifanya mazoezi ya kusoma
hotuba hiyo nilikuwa nikiumia, lakini niliumia zaidi wakati alipokuwa jukwaani
akiisoma nilipogundua kuwa kumbe si mimi tu ninayeumizwa na historia ya
kusikitisha ya Ray C baada ya kuangalia viongozi meza kuu wengi wakifutaa
Machozi, nilipoangalia upande mwingine kwa watazamaji niliona watu hapa na pale
wakifuta machozi.
Katika muda Mfupi niliokuwa nikimsadia nilijifunza jambo moja
kubwa kwamba vijana wengi sana wamevutiwa na Ray C na wanamsikiliza. Walikuwa
wakitusikiliza kwa namna ya kipekee sana na kila siku idadi ya vijana waliokuwa
tayari kuacha dawa ilikuwa ikiongezeka kwa kasi ya ajabu kutokana na hamasa
tuliyokuwa tukiwapa.
Huko kwenye shule za sekondari wanafunzi walifurahi na katika
mahojiano yam mmoja mmoja walikiri kupata ufunuo mpya na muhimu katika maisha
yao. Jambo hili linanivuta leo kufikiria kama kweli Serikali inakusudia kueneza
elimu ya athari ya madawa ya kulevya basi Ray C aweza kuwa chombo kizuri cha
kufanikisha hilo. Mimi naamini gharama zinazotumika ni kubwa sana lakini
ufanisi wake ni mdogo mno, lakini kwa kumtumia Ray C gharama hizo zaweza kuwa
na ufanisi mkubwa kupindukia.
Kama mashirika ya simu, shirika la chakula nk yanakuwa na utaratibu
wa kuwa na balozi wa huduma za mashirika hayo basi nadhani ni wakati muafanya
wa kumteua Ray C kuwa balozi katika maapambano dhidi ya madawa ya kulevya hasa
katika uelimishaji jamii. Kuna mafungu mengi yanatengwa kwenye Serikali na
wanalipwa watu ambao kazi zao hazina mchango mkubwa sana kwa Taifa, Serikali ifanye
sasa hivyo kwa mtu ambaye ushiriki wake utapanua ufanisi wa malengo ya Serikali
kwa kasi kubwa.
Nasema haya kwasababu mimi mwenyewe nimeshuhudia hamasa kubwa
ambayo vijana walikuwa wakipata tulipokuwa kwenye kampeni zetu.
Mungu Ibariki Tanzania
Kwa maoni: malihoja@yahoo.com
No comments:
Post a Comment